Watoto 170 waliuawa kila siku Nigeria kutokana na mizozo

Maelezo ya sauti, Watoto 170 waliuawa kila siku Nigeria kutokana na mizozo

Umoja wa Mataifa unasema takriban watoto 170 walikufa kila mwaka jana kutokana na mizozo kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Katika ripoti mpya kuhusu jinsi uasi unayoathiri watu katika kanda hiyo, shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa maendeleo UNDP limesema huenda Nigeria ikawapoteza zaidi ya watoto milioni moja ifikapo mwaka 2030 iwapo mzozo huo wa kaskazini mashariki mwa Nigeria utaendelea.

Kulingana na ripoti hiyo, idadi ya watoto wanaofariki dunia kila siku katika eneo hilo huenda ikaongezeka hadi 240 ifikapo mwaka 2030 na kuongeza wanaothirika zaidi na mizozo inayosababishwa na uasi wa makundi yenye itikadi kali. Ni watoto wa chini ya umri wa miaka mitano ambao wako katika hatari zaidi ya kukumbwa na utapia mlo na magonjwa yatokanayo na ukosefu wa maji safi.

Mbali na kukosa mahitaji ya kimsingi kutokana na kulazimika kuyahama makazi yao, ukosefu wa huduma za kutosha za afya kunasalia kuwa sababu kuu uya watoto kupoteza maisha katika maeneo ya mizozo.

UNDP pia inakadiria kuwa takriban wanafunzi milioni moja na laki nane wameacha masomo katika kanda hiyo kutokana na mzozo unaoendelea.

Shirika hilo limesema hali ni mbaya mno na inahitaji hatua za dharura kutoka kwa jumuiya ya kimataifa na serikali kuwasaidia watu wa kaskazini mashariki mwa Nigeria.