Mkulima mstaafu ambaye sauti yake inawafanya watu wakabiliane na hofu
Watu kutoka maeneo mbali mbali duniani wamemshukuru mkongwe wa miaka 84 nyota wa YouTube ambaye sauti yake inawasisimua , kuwafurahisha na kuwafanya wakabiliane na hofu. John Butler alikuwa nyota ambaye hakutarajiwa wakati mahojiano aliyoyafanya mwaka 2016 yalipokuwa maarufu kwa jamii ya watu wanaohisi hisia za msisimko na za ganzi mwilini mwao zinazofahamika kama (Autonomous Sensory Meridian Response (ASMR). Watu wanaopata hisia hizi huhisi wamepumzika, na mara nyingi hupata hisia za kutuliza ambazo huwa zinasambaa mwilini mwao. Mkulima huyu mkongwe mstaafu ambaye anazungumza kwa sauti laini amewavutia mamilioni ya watazamaji na zaidi ya 120,000 wamejisajiri kwenye video za falsafa yake kuhusu maisha na tafakari.
