Kituo cha redio cha Al-Shabaab cha shambuliwa

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Taarifa kutoka nchini Somali zasema kuwa kituo cha redio cha wanamgambo wa Alshabab cha Al-Andalus kimevamiwa kwa shambulio la anga jana usiku katika wilaya ya Kuntuwarey eneo la Shabelle.

Kulingana na tovuti za wanaounga mkono wanamgambo hao, shambulio hilo limesababisha watu watatu kujeruhiwa katika nyumba iliyo mkabala na jengo la kituo hicho cha redio ambalo limeharibika vibaya.

Inaaminika kuwa shambulio hilo la anga limetekelezwa kwa kutumia ndege isiyokuwa na rubani.

Hadi kufikia sasa mkuu wa jeshi la Marekani barani Afrika hajasema lolote kuhusiana na shambulio hilo ingawa nchi hiyo imetekeleza mashambulizi kadhaa nchini Somalia katika miaka ya hivi karibuni.

Aidha serikali ya Somali pia nayo haijasema lolote juu ya shambulio hilo lililotokea eneo la Kuntuwarey.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Marekani imekuwa ikiimarisha mashambulizi yake nchini Somalia tangu Rais Donald Trump alipoingia madarakani.

Mwaka wa kwanza Bwana Trump kuingia madarakani, ndege zisizo na rubani za Marekani zilifanya mashambulizi 27 dhidi ya kambi za Al-Shabaab na wanachama wa kundi hilo nchini Somali.

Wakati huohuo, wanajeshi wa Marekani nchini Somali wanatoa mafunzo na ushauri kwa jeshi la nchi hiyo.

Somalia

Chanzo cha picha, AFRICOM

Jeshi la Marekani nchini Somali pia linashirikiani na vikosi vya Umoja wa Afrika nchini humo (AMISOM

April 2019, Rais Trump alitia saini amri ya rais kuliko muwezesha kuongeza muda wa vikosi maalum vya Marekani nchini Somalia kwa mwaka mmoja zaidi.

Hata hivyo, hata kama pengine kuongezwa muda kwa wanajeshi wa Marekani nchini Somalia huenda ikawa ni mara ya mwisho, maafisa wa ulinzi wa Marekani wanasema huenda oparesheni zake nchini humo zikaendelea kwa miaka kadhaa.

Kwa kipindi cha zaidi ya miaka mitatu sasa, ujumbe maalum wa Marekani umekuwa nchini Somalia majukumu yake makuu ikiwa kusaidia serikali ya Somalia katika nyanja kadhaa kama vile:

  • kukabiliana na wanamgambo wa Al-Shabaab.
  • kutoa ushauri wa utekelezaji wa mashambulio ya anga na ardhini.
  • kutoka mafunzo ya kijeshi.
  • Na kuimarisha uwezo wa jeshi la nchi hiyo.