Virusi vya Corona: Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli kutuma ndege Madagascar kuchukua 'dawa ya corona'

Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania

Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli leo Jumapili Mei 3 amesema atatuma ndege Madagascar kwenda kufuata dawa ya mitishamba ambayo rais wa nchi hiyo anadai kuwa inatibu corona.

Magufuli amesema kuwa amewasiliana na Madagascar baada ya kupokea barua rasmi kutoka nchi hiyo iliyoeleza kuwa wamegundua dawa ya corona.

"Ninawasiliana na Madagascar na wameshaandika barua. Wanasema kuna dawa zimepatikana kule, tutatuma ndege kule na dawa zile zitaletwa pia ili Watanzania nao waweze kufaidika nayo… Sisi serikali tupo tunafanya kazi usiku na mchana."

coronavirus

Rais Magufuli ameyasema hayo hii leo katika hafla fupi ya kumwapisha Mwigulu Nchemba kuwa Waziri wa Katiba na Sheria akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Balozi Augustine Mahiga aliyefariki Ijuumaa.

Hata hivyo, shirika la Afya Duniani (WHO) limeonya juu ya ubora wa dawa hiyo ambayo ni kinywaji kilichotengenezwa kwa mitishamba.

Matunda, ndege, mbuzi wakutwa na corona

Wakati huo huo, rais Magufuli amesema pia sampuli kadhaa ambazo hazikuwa za binadamu zilitumwa katika maabara ya taifa hilo ili kupima ubora na usahihi wa majibu ya mashine hizo katika vipimo vya ugonjwa huo.

''Sampuli hizo zilipewa majina ya binadamu na kupelekwa bila ya wataalamu wa maabara kujua kuwa si za bidanamu'', ameeleza Magufuli.

Sampuli ya oili ya gari ilipewa jina la Jabiri Hamza na haikukutwa na corona. Sampuli ya Tunda la fenesi ilipewa jina la Sara Samuel majibu yake hayakukamilika, sampuli ya papai iliitwa Elizabeth na kukutwa na corona.

Sampuli ya ndege kwale pia ilikutwa na corona pamoja na mbuzi pia.

"…Lazima ugundue kuna mambo ya ajabu yanafanyika nchi hii. Ama wahusika wa maabara wamenunuliwa na mabeberu, ama hawana utaalamu jambo ambalo si kweli kwa kuwa maabara hii imetumika sana katika magonjwa mengine. Ama zile sampuli zinazoletwa maana vifaa vyote vinatoka nje, hivyo lazima kuna kitu fulani kinafanywa," amesema Magufuli.

Magufuli amesema kutokana na taarifa hizo anaamini kuna watu ambao walipewa majibu yasiyo sahihi.

"Lazima kuna watu wameambiwa positive lakini si wagonjwa wa corona, na inawezekana wengine wakafa kwa hofu. Papai lile lipo halijafa linaiva tu. Mbuzi yule yupo tu hajafa, fenesi lile lipo tu labda lije kuoza…kwa hiyo natoa wito kwa Watanzania msiwe na hofu…mbona mafua yamekuwepo lakini haya ni makali, nayo yatapita..."

Jinsi chanjo ya corona itakavyofanya kazi
Maelezo ya picha, Jinsi chanjo ya corona itakavyofanya kazi

Kutokana na hilo, Magufuli amemwagiza waziri Nchemba kwenda kufanya uchunguzi katika maabara hiyo na endapo kutakuwa na jambo lolote la jinai litakalogundulika basi hatua zichukuliwe.

Magufuli pia ametaka uchunguzi zaidi kwa nchi za Afrika na WHO juu ya sampuli na ubora wa vifaa vya kupimia maradhi hayo.

Kuhusu wanyama kukutwa na corona, nchini Marekani paka wa kufugwa nyumbani, simba na chui wa kufugwa kwenye mabustani pia wamekutwa na virusi hivyo.

Waliofunga makanisa na misikiti washutumiwa

Magufuli pia ameshutumu vyombo vya habari vya kimataifa kwa namna vinavyoripoti kuhusu janga hilo nchini Tanzania licha ya kuwa vipo katika maeneo ambayo yaneathirika zaidi.Pia amewashutumu viongozi wa dini ambao wamefunga nyumba za ibada na kuwasifu wale wanaoendelea na ibada misikitini na makanisani katika kipindi hiki. Kuhusu wapinzani kususia vikao vya Bunge Dodoma amesema ameshatoa maelekezo kuwa wasilipwe posho zao na kuwatuhumu kwa kutumiwa na mabeberu. Katika hatua nyengine, rais Magufuli amesema anafikiria kuruhusu ligi ya mpira iendelee hata kwa kuoneshwa kwenye runinga na anasubiria ushauri wa wataalamu wake kabla ya kulifanyia uamuzi jambo hilo.

Matamshi yake yanajiri baada ya rais wa Madagascar Andry Rajoelina kutangaza kwamba taifa lake limezindua dawa ya mitishamba ya kutibu Covid-19.

Rais aliwataka watafiti kuja na tiba ambayo 'waliipata kwamuda muafaka'

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Rais aliwataka watafiti kuja na tiba ambayo 'waliipata kwamuda muafaka'

WHO yapinga utumizi wa tiba ya kibinafsi kutibu corona

Ikizinduliwa kwa jina Covid-Organics, dawa hiyo ilitengenezwa kutoka kwa mmea artemisia (pakanga) - ambao ni mojawapo ya miti ambayo huchanganywa pamoja na mimea mingine ya Madagascar kama tiba ya ugonjwa wa Malaria.

Dawa hiyo ambayo imepakiwa kwenye chupa na kutangazwa kama chai ya miti shamba ilifanyiwa majaribio miongoni mwa watu wasiozidi 20 kwa kipindi cha wiki tatu, kulingana na katibu wa rais huyo Lova Hasinirina Ranoromaro aliyezungumza na BBC.

"Vipimo vimefanyika-watu wawili wamekwishapona kutokana na tiba hii," Bwana Rajoelina alisema katika uzinduzi wa Covid-Organics uliofanyika katika taasisi ya utafiti ya Madagascar- Malagasy Institute of Applied Research (Imra), ambayo ndiyo iliyotengeneza dawa hiyo ya mitishamba.

Rais Rajoelina ametaka wanafunzi wapewe kinywaji hicho kwa kiwango kidogo kila baada ya muda kwa siku.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Rais Rajoelina ametaka wanafunzi wapewe kinywaji hicho kwa kiwango kidogo kila baada ya muda kwa siku.

"Kinywaji cha dawa hii ya mitishamba huonesha matokeo katika kipindi siku saba," alisema rais huyo mwenye umri wa miaka 45, ambaye aliwataka watu kuitumia kama hatua ya kujikinga na ugonjwa wa corona.

"Watoto wa shule wanapaswa kupewa kinywaji ... kidogo kidogo kwa siku nzima," aliwaambia mabalozi na watu wengine waliokua wamekusanyika kwa ajili ya uzinduzi wa kinywaji hicho.

Maelezo ya video, Coronavirus: Utajuaje kuwa umeathirika na virusi?

Lakini ikizungungumzia uzinduzi wa Covid-Organics, WHO imeambia BBC kwamba shirika hilo la dunia halishauri "matibabu ya kibinafsi ya dawa zozote... kama njia ya kinga au tiba ya Covid-19."

Lilirejelea kauli za mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus kwamba "hakuna njia za mkato" za kutafuta dawa ya kupambana na virusi vya corona.

Majaribio ya kimataifa yanaendelea kupata tiba yenye ufanisi , WHO iliongeza.

Ramani

Maambukizi yaliyothibitishwa duniani

Group 4

Weka taarifa mpya tafadhali

Chanzo: Chuo kikuu cha Johns Hopkins (Baltimore, Marekani), maafisa wa eneo

Idadi ya hivi karibuni 5 Julai 2022 08:59 GMT +1

Tunaendelea kukupasha zaidi...