Rais wa Rwanda Paul Kagame avishutumu vikosi vya Burundi kushambulia DRC

Chanzo cha picha, LIVE EVENT
Rais wa Rwanda Paul Kagame amevishutumu vikosi vya Burundi kuendesha mapigano mashariki mawa Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, huku akipinga madai kuwa wanajeshi wa Rwanda wako katika eneo hilo pia.
Jimbo la Kivu Kusini katika Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Kongo linakabiliwa na mzozo wa kivita kwa sasa baina ya makundi mengi ya eneo hilo pamoja na waasi wa Burundi na Rwanda wanaopinga serikali za Bujumbura au Kigali.
Akizungumza na waandishi wa habari, rais wa Rwanda Paul Kagame amesema majeshi ya Burundi ndio yako katika eneo hilo la Kivu Kusini.
Maelfu kwa maenlfu ya watu wamelazimika kukimbia makazi yao kutokana na mapigano makali ya kijeshi yanayoendelea ambayo yamechacha katika siku za hivi karibuni
Wakazi na baadhi ya mashirika yasiyokuwa ya kiserikali (NGO's) yanadai majeshi ya Rwanda na ya Burundi yanapigana sambamba na makundi ya wanamgambo katika mizozo inayoendelea.
Katika mkutano kwa njia ya video na waandishi wa habari Jumatatu, Bwana Kagame aliwaambia waandishi wa habari kuwa baadhi ya mashirika yasiyokua ya kiserikali na wataalamu hawaangalii kile kinachoendelea pale, bali wanataka kuona uwepo wa wanajeshi wa Rwanda.
"Intelijensia yetu inatuambia kwamba tunavikosi kutoka Burundi,vikosi vya serikali, vinavyoendesha hatrakati zake katika jimbo lile.
" Hakuna mwanajeshi hata mmoja wa Kikisi cha ulinzi cha Rwanda (Rwandan Defense Force) ambaye amekwenda katika eneo lile...(na) wanajeshi wa DRC na serikali ya DRC wanafahamu ukweli kwamba hakuna askari wa RDF aliyeko pale" alisema Bwana Kagame.

Chanzo cha picha, AFP
Amesema kuwa Wanyarwanda walioko huko ni wapiganaji wanaoipinga serikali ya Rwanda wa kundli la FDLR na makundi mengine yanayounga mkono wapiganaji hao.
Bwana Kagame amesema jambo zuri kwa sasa ni kwamba serikali ya sasa ya Kongo inakubali kushirikiana na nchi jirani katika kutatua tatizo la mika mingi la wapiganaji wa msituni.
Mwezi Oktoba mwaka jana wanajeshi DRC walianza harakati za kuyamaliza makundi yenye silaha katika maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo, licha ya kwamba harakati hizo hazionekani kuzaa matunda.
Akijibu kuhusu shutuma za rais wa Rwanda msemaji wa rais wa Burundi Jean Claude Karerwa amekana uwepo wa wanajeshi wa Burundi mashariki mwa DRC.
Katika ujumbe wake alioutuma kwa BBC, Bwana Karerwa alisema: "Labda iombwe na AU au Umoja wa Mataifa, vinginevyo Burundi haiwezi kupeleka wanajeshi wake katika taifa jingine ".
Uhasama kati ya Burundi na Rwanda umekuwepo
Serikali za Burundi na Rwanda zimekua na uhasama tangu mwezi Mei, 2015 wakati lilipofanyika lililofeli la mapinduzi dhidi ya rais wa Burundi Pierre Nkurunziza na baadhi ya waandalizi wa jaribio hilo kukimbilia Rwanda.
Burundi ilidai kwamba Rwanda iliwafadhili waliohusika na kwamba inatoa hifadhi kwao. Rwanda mara kwa mara imekuwa ikikanusha tuhuma hizo.
Mwaka jana Rais Nkurunziza alimwandikia barua Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Yoweri Museveni wa Uganda akisema Rwanda sasa si mshirika tena ndani ya jumuiya bali ni kama adui.
Kiongozi huyo alitaka kufanyike mkutano maalum wa EAC wa kujadili mzozo huo kati ya Rwanda na Burundi, jambo ambalo halikuzaa matunda.
Usafiri baina ya nchi hizo mbili ulifungwa na hivi karibuni Rwanda ilitangaza kuwa Burundi imekataa kuruhusu shehena na magari ya mizigo yanayotoka Uganda na Kenya yanayopitia Rwanda kuingia nchini Burundi.
Serikali ya Rwanda pia iliwasihi wananchi wake walioko karibu na mpaka kati ya nchi hiyo na nchi ya Burundi kusitisha biashara yoyote na majirani zao wa nchi ya Burundi.














