Omar Al Bashir aandamwa na mashtaka ya mauaji

Chanzo cha picha, AFP
Mwendesha mashtaka wa umma nchini Sudan amemshitaki rais aliyeondolewa madarakani Omar al-Bashir kwa makosa ya kuchochea na kuhusika na mauaji ya waandamanaji.
Mashtaka hayo yametokana na uchunguzi uliofanywa kuhusu kifo cha ddaktari aliyeuawa wakati wa maandamano yaliyosababisha kumalizika kwa utawala wake mwezi uliopita.
Hatma ya Bwana Bashir haijawa wazi. Aliripotiwa kutiwa nguvuni mara baada ya kupinduliwa.
Anakabiliwa pia na uchunguzi juu ya madai ya wizi wa pesa na kudhamini ugaidi.

Chanzo cha picha, Reuters
Baadhi ya watu wa Sudan hawawezi kuamini kuwa Bwana Bashir kweli yuko mashakani kutokana na uhalifu wa aina hiyo mpaka watakapomuona akiwa mahakamani, ameripoti mwandishi wa BBC Will Ross.
Mnamo mwezi Disemba, waandamanaji walianza maandamanano dhidi ya uamuzi wa serikali wa kupandisha mara tatu kwa bei ya mkate.
Maandamano hayo ghafla yalibadilika kuwa hasira iliyosambaa kote nchini dhidi ya kiongozi huyo ambaye alikuwa mamlakani kwa miaka 30, yakiongozwa na madaktari.
Maandamano yalifanyika kwa wiki tano na shahidi mmoja anasema tarehe 17 Januari, vikosi vya usalama viliwafyatulia risasi waandamanaji na kumuua daktari.
Alikuwa akiwatibu waandamanaji waliokuwa wamejeruhiwa nyumbani kwake mjini Khartoum wakati polisi walipofyatua gesi za kutoa machozi katika jengo lake.
Mtu mmoja aliyeshuhudia tukio hilo aliiambia BBC kwamba daktari alikuwa ametoka nje ya nyumba yake huku akiwa ameinua mikono yake juu ,akawaambia polisi kuwa yeye ni daktari , lakini walimpiga risasi mara moja.

Chanzo cha picha, AFP
Daktari huyo ni mmoja wa watu makumi kadhaa waliouawa wakati wa maandamano ya kuipinga serikali.
Baadaye waandamanaji waliamua kufanya maandamano yao kuwa kuketiu nje ya makao makuu ya kijeshi, na kudai jeshi limg'oe mamlakani rais.
Baraza la kijeshi lilichukua mamlaka ya nchi tarehe 11 Aprili, lakini waandamanaji wanasisitiza kwamba jeshi lazima likabidhi utawala wa nchi kwa raia.
Mazungumzo kati ya jeshi na muungano wa upinzani yamekuwa yakiendelea ili kubuni baraza la mpito la utawala wa pamoja litakaloongoza nchi.












