Aliyekuwa Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad ametangaza kuhamia ACT.

Maelezo ya sauti, Aliyekuwa Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad ametangaza kuhamia ACT.

Aliyekuwa Katibu mkuu wa chama cha CUF Maalim Seif Sharif Hamad amesema hatua ya mahakama inadhihirisha wazi ni mipango ya vyombo vya Serikali kukihujumu na kukidhohofisha chama cha CUF.

''Tumeshuhudia Serikali kupitia vyombo vyake, kama Ofisi ya msajili wa vyama vya siasa, wakala wa usajili, udhamini na Ufilisi, lakini pia Polisi, Bunge na Mahakama kuwa sehemu ya mkakati huu''.AlielezaMaalim Seif Sharif Hamad baada ya Mahakama nchini Tanzania kutoa hukumu dhidi ya kesi namba 23 ya mwaka 2016.

Kesi hiyo ilifunguliwa kupinga uamuzi wa msajili wa vyama vya siasa, kuingilia maamuzi ya ndani ya chama, pale alipomtambua Profesa Ibrahim Lipumba kuwa mwenyekiti wa CUF, pamoja na kuwa alijiuzulu na mkutano wa taifa wa chama kuridhia kujiuzulu .

Maalimu Seif amesema kuahirishwa kusomwa kwa kesi hiyo kutoka tarehe 22 mwezi Februari hadi tarehe 18 Mwezi Machi kulikua na lengo la kutoa nafasi kuwa upande aliodai kuwa ulikua ukibebwa na dola ili kuandikisha tena bodi yao ya wadhamini na kufanya mkutano mkuu ili wakati uamuzi unatolewa uwe umewaingiza katika mgogoro mwingine.

''Labda lengo ni kutufanya tuendelee kupanda na kushuka mahakamani huku tukishindwa kufanya shughuli za kisiasa.'sasa imetosha' mapambano lazima yaendelee''.Alisema Maalim Seif huku akishangiliwa na wafuasi wake.