Tundu Lissu: Tumeingia kipindi cha giza nene la utawala wa kidikteta Tanzania

Maelezo ya video, Tundu Lissu: Tumeingia kipindi cha giza nene la utawala wa kidikteta Tanzania

Mwanasiasa wa upinzani Tanzania ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu amekuwepo nchini Ubelgiji kwa ajili ya kupata matibabu tangu kupigwa risasi na watu wasiojulikana mwaka jana.

Katika mahojiano na BBC amezungumzia hali inayowakabiliwa wanasiasa wa upinzani nchini humo.

Katika mazungumzo yake na mwandishi wetu Zuhura Yunus amezungumzia hali ya upinzani nchini Tanzania.

Kwa mujibu wake, upinzani unakabiliwa na wakati mgumu sana chini ya utawala wa Rais Dkt John Magufuli.

"Wapinzani hatujakaa kimya, ... viongozi wa upinzani wanapigania maisha yao, tuna familia. Huwezi kama unaambiwa uwe mahakamani kila siku ili ujitetee, huo muda wa kwenda kufanya kazi nyingine unakuwa haupo. Lakini kusema kweli hatujanyamaza, lakini ukatili ambao tunakabiliana nao ni mkubwa sana,” amesema.

Hata hivyo, amesema ana mpango wa kurejea Tanzania na kuendelea na majukumu yake kama mbunge punde atakapopewa ruhusa na daktari.

Lissu anasema pia bunge la Tanzania halijajikimu kulipa gharama za matibabu yake tangu alazwe hospitalini.

Hata hivyo serikali kwa upande wake imeeleza kuwa Bwana Lissu hakufuata utaratibu unaotakiwa wa kupelekwa kwanza katika hospitali ya taifa ya Muhimbili ili aweze kuandikiwa mapendekezo ya kupelekwa na kutibiwa nje ya nchi au katika hospitali nyingine.

Spika wa Bunge la Tanzania Job Ndugai ameiambia BBC Dira ya Dunia kwamba iwapo utaratibu huo utafuatwa hata sasa, malipo ya huduma zote za matibabu zitalipwa na bunge la Tanzania.

Unaweza kusoma pia: