Magufuli: Serikali haikusababisha tetemeko Kagera

Chanzo cha picha, Ikulu, Tanzania
Rais wa Tanzania John Magufuli amewasihi Watanzania kuwapuuza watu aliosema wanataka kutumia maafa yaliyotokana na tetemeko la ardhi eneo la Kagera kuchochea chuki dhidi ya serikali.
Mikoa jirani ya Mwanza, Geita na Mara pia iliathirika.
Dkt Magufuli amesema hata mataifa makubwa yenye maendeleo makubwa ya uchumi na teknolojia yanakumbwa na mitetemeko ya ardhi na kusababisha vifo vya idadi kubwa ya wananchi na uharibifu mkubwa wa mali.
Akiongea mwishoni mwa wiki, rais huyo alisema mpaka sasa hakuna teknolojia ya kutabiri kutokea kwa tetemeko la ardhi na kwamba tetemeko hilo halikuletwa na serikali.
"Nilikuwa najaribu kuangalia kwa mfano nchi kama China kwenye mwaka 2014 watu 617 walipoteza maisha, mwaka 2013 walipoteza watu 193, Mwaka 2010 walipoteza watu 2,998 mwaka 2008 China ilipoteza watu 98,712," alisema kwa mujibu wa taarifa kutoka ikulu.
"Ukijaribu kuangalia Japan, nchi ambayo imeendelea na ina utaalamu wa hali ya juu sana, kwenye mwaka 2016 tarehe 14 mwezi wa nne ilipoteza watu 6, baada ya siku mbili tarehe 16 mwezi wa nne 2016 tetemeko likatokea tena na likaua watu 35 … mwaka 1923 liliua watu 142,800 na hiyo ni Japan."
Rais Magufuli alisema hayo Jumamosi katika ikulu ya Dar es Salaam alipokuwa akipokea mchango wa fedha taslimu kiasi cha Dola za Kimarekani laki mbili (Tshs 437 milioni) kutoka kwa Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni kusaidia walioathiriwa na tetemeko hilo lililotokea wiki moja iliyopita.

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta alituma mchango wa mabati, blanketi na magodoro vyenye thamani ya shilingi za Kitanzania milioni 115 kuwasaidia waathiriwa.
Watu 17 walifariki, 440 wakajeruhiwa na nyumba 2,063 zikabomoka kutokana na tetemeko hilo kwa mujibu wa serikali ya Tanzania.
Nyumba 14,081 zipo katika hali hatarishi na nyumba 9,471 zimepata uharibifu mdogo, huku watu 126,315 wakihitaji misaada mbalimbali.

Rais Magufuli ameahidi kuwa Serikali itahakikisha inarekebisha miundombinu iliyoharibika lakini akawataka wananchi wajipange kurekebisha nyumba zao kwa kuwa Serikali pekee yake haitaweza kujenga nyumba zote zilizobomoka.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa, kufikia mwishoni mwa wiki shilingi za Kitanzania bilioni tatu nukta sita (dola 1.6 milioni) zilikuwa zimepatikana za kuwasaidia waathiriwa.













