Mji wa ajabu, wa zama za Soviet uliojengwa juu ya meli zilizozama

Muonekano wa juu wa jiji kubwa la Neft Dashlari linaloelea, maili 48 katika picha ya 1997.

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 6

Katikati ya Bahari ya Caspian, kisiwa, kilichojengwa kwa mkono wa mwanadamu - minara ya chuma ya kustaajabisha, mabomba, madaraja ya mbao, majengo ya kutoka enzi ya Soviet - ambayo hayaonekani kwenye ramani: Karibu Neft Dashlari.

Historia yake ilianza miaka ya 1940, wakati Joseph Stalin aliamuru ujenzi wa eneo hili baada ya kugundua kuwa kulikuwa na mafuta chini ya bahari ya Caspian.

Iko kilomita 55 kutoka Baku, kwenye mwambao wa Azerbaijan, na jina lake kwa Kirusi linamaanisha "Miamba ya Mafuta" au, kama inavyojulikana kwa Kiingereza,"Oil Rocks",kwa sababu jiji hili ni la zamani zaidi katika pwani. Eneo lenye mafuta ulimwenguni, kulingana na Kitabu cha rekodi cha Guinness.

Ni mjini Baku ambapo Kongamano la 29 la Umoja wa Mataifa la Mabadiliko ya Tabianchi mwaka 2024, COP29, litafanyika wiki ijayo.

Mji kwenye meli zilizozama

Ilikuwa 1920 ambapo Jeshi la kisovieti liliingia Azerbaijan na kuichukua kama sehemu ya USSR (Muungano wa Soviet). Ilikuwa chini ya USSR hadi Oktoba 1991, muda mfupi kabla ya kuvunjika kwake rasmi.

Wakati wa Vita vya pili vya dunia, ilikuwa muhimu kwa mkakati wa nishati wa Urusi, kwani mafuta mengi yaliyotumiwa na kambi ya Mashariki yalitoka Baku.

Hapo awali Neft Dashlari iliundwa kama sehemu ya mradi wa miaka mitano uliosimamiwa na Stalin, ambayo ni, miradi ya miaka mitano ya maendeleo ya uchumi wa Soviet, ambayo ilikuwa alama ya usimamizi wa Soviet, ingawa mingi haikukamilishwa kutokana na kuachwa au kushindikana.

Ujenzi wake ulianza baada ya uchunguzi wa kwanza wa mafuta uliofanikiwa mnamo Novemba 7, 1949. Eneo hilo liligeuka kuwa moja ya hifadhi kubwa zaidi ya mafuta katika Asia ya Kati.

Awali kilikuwa jukwaa dogo la uchimbaji na nyumba ndogo kwa wafanyikazi kukaa hapo,na kubadilika kuwa ujenzi mkubwa kuanzia 1951.

Chanzo cha picha, SOCAR

"Mnamo Novemba 7, kisima hicho kilitoa mafuta mengi (tani 100 kwa siku), kuashiria uzalishaji wa kwanza wa mafuta. Azerbaijan ndiyo ya kwanza kuchimba mafuta katika sehemu ya wazi ya Bahari ya Caspian,” kwa mujibu wa tovuti ya SOCAR, kampuni ya mafuta ya serikali ya Azerbaijan.

Kile ambacho awali kilikuwa eneo ndogo la uchimbaji na nyumba ndogo kwa ajili ya wafanyakazi kukaa huko, ilibadilika kuwa ujenzi mkubwa kutoka 1951. "Muujiza wa usanifu na kiufundi", alisema mtengenezaji wa filamu Marc Wolfensberger alistaajabia alipoweza kupaona mwishoni mwa Miaka ya 1990.

Ili kuharakisha ujenzi wa eneo hilo la pwani, jambo lisilo la kawaida lilifanyika: meli zilizokataliwa zilizamishwa ili kuzitumia kama msingi huku juu yake nguzo za majengo zilisimikwa.

Miamba ya mafuta hapo awali ilijengwa kama sehemu ya mpango wa miaka mitano uliosimamiwa na Stalin.

Chanzo cha picha, Getty Images

Moja ya meli hizi ilikuwa meli ya mafuta ya Zoroaster, ya kwanza kuwahi kutengenezwa duniani. Muundaji wake, Ludvig Nobel - kaka wa Albert Nobel – alitengeneza kama suluhisho la kusafirisha mafuta mwishoni mwa karne ya 19.

"Mnamo 1951, ili kulinda kisiwa hicho kutokana na upepo na mawimbi, meli sita za ziada za kampuni za Khazartanker na Khazardonanma zilibomolewa na kuletwa hapa zikiwa zimezama nusu, na ghuba ya bandia iliundwa kuzunguka kisiwa hicho.

Vyumba vya kuhifadhia meli vilitumika kama ukumbi wa maakuli ,kituo cha matibabu, sehemu za kulala, na matumizi mengine kwa wafanyikazi wa kuchimba visima.

Hapa ndipo asili ya jina la mahali hapa, "Kisiwa cha Meli Saba" lilipotokea," tovuti ya SOCAR inasema.

Baadaye, kisiwa hiki cha bandia kilijulikana kwa jina lake la sasa.

Mahali pa kuishi

Kwa miaka mingi, Neft Dashlari ilipanuka na kuwa jiji kubwa mfano wa umbo la pweza kwenye bahari.

Vitalu vya ujenzi kwa wafanyikazi, duka la mikate, maduka, vituo vya matibabu, uwanja wa mpira wa miguu, helikopta na hata ukumbi wa michezo.

Leo, Mirvari Gahramanli, mkurugenzi wa Shirika la Kulinda Haki za Wafanyakazi wa Mafuta, ambalo linaangazia haki za binadamu katika sekta ya mafuta na gesi ya Azerbaijan, anaiambia BBC Mundo, Neft Dashlari imejengwa mita kadhaa juu ya uso wa bahari juu ya nguzo za chuma zilizowekwa chini ya bahari.

Na, anasema, majengo haya ya makazi, idara ya matibabu na usafi na maduka bado yapo. Isitoshe, “miti imepandwa kwenye vizimba vya chuma na bustani zitengenezwa”

Kisiwa cha kwanza cha aina yake

‘’Hifadhi ya Neft Dashlari inachukuliwa kuwa ya kwanza kuchimbwa katika bahari ya wazi duniani. Na mahali hapa, kwa sababu ya upekee wake, wakati mwingine huitwa maajabu ya nane ya ulimwengu, kisiwa cha meli saba, kisiwa cha maajabu, "anasema Gahramanli.

Eneo la oil rocks lina urefu wa kilomita 12 na upana wa kilomita 6 na, kulingana na data za Gahramanli, takriban visima 2,000 na karibu kilomita 200 za njia za juu zimechimbwa katika eneo hilo.

Hapo mwanzo, kisiwa kilikuwa na wafanyikazi wapatao 5,000. Leo, kwa mujibu wa Gahramanli, kuna wafanyikazi wapatao 3,000 ambao hutumia siku 15 baharini na siku 15 kwenye nchi kavu.

Jengo la makazi la Neft Dashlari, katika picha kutoka kampuni ya mafuta inayimilikiwa na serikali SOCAR ilichapishwa katika ukurasa wa mtandao wa X wa serikali ya Azerbaijan

Chanzo cha picha, SOCAR

Neft Dashlari ni kampuni inayomilikiwa na SOCAR, kampuni ya mafuta inayomilikiwa na serikali ya Azerbaijan inayojishughulisha na uzalishaji, usindikaji na usafirishaji wa mafuta, na gesi pamoja na uuzaji wa bidhaa za mafuta, gesi.

Kwa mujibu wa SOCAR, kisiwa hicho kilikuwa na manufa amakubwa katika uzalishaji wa mafuta ya Caspian na kimezalisha karibu tani milioni 180 za mafuta katika miaka 75 ya kuwepo kwake.

Katika kilele chake mnamo 1967, ilivuka rekodi ya tani milioni 7.6.

Leo, uzalishaji wa mafuta kila siku uko chini, karibu tani 3,000, kulingana na takwimu zilizotolewa na SOCAR kwa kipindi cha Januari mwaka huu.

Kuanza kuharibika

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kisiwa hicho kilidumu haswa katika miaka ya 1960. Lakini kuanzia muongo uliofuata, kutokana na kubadilika-badilika kwa bei ya mafuta na kuanza kuporomoka kwa dola ya kisovieti, fahari yake ilianza kupungua.

Kwa mujibu wa gazeti la Ujerumani Der Spiegel, ni kilomita 45 tu kati ya 300 za barabara zilizoweza kupitika mwaka wa 2012.

Katika filamu ya Oil Rocks - City Above The Sea, mtayarishaji filamu Marc Wolfensberger ananasa baadhi ya nyakati za kudhoofika huku.

“Barabara hizi zote zilikuwa katika hali nzuri nilipokuwa mtoto,” anasema mfanyakazi wa eneo hilo akiwa katika lori. Picha inayofuata ni ya majengo yaliyotelekezwa , yaliyoharibiwa na yenye kutu.

Alipoulizwa kuhusu hatari ya kisiwa hicho kuzama, kutokana na muundo wake au mabadiliko ya hali ya hewa, Mirvari Gahramanli anasema: “ Kisiwa hakiko karibu kuzama na hakuna hatari kama hiyo kwa sasa.

Neft Dashlari ni kituo cha kimkakati kilichoko baharini. Kuna bahari na visima. Mafuta yanachimbwa huko, uchimbaji, ujenzi, mitambo n.k.

Picha ya muonekano wa moja kati ya majengo ya makazi katika kisiwa cha Neft Dashlari.Iliyopigwa 1997

Chanzo cha picha, Getty Images

Sio rahisi kupata picha za hivi karibuni za kisiwa hicho

Kwa kudadisi tu, tovuti ya SOCAR inajumuisha filamu zote zilizotengenezwa katika eneo hilo, zikiwemo "The world is not enough" iliyotayarishwa na kampuni ya James Bond mwishoni mwa miaka ya 90.

Ingawa inawezakana kufika kwa helikopta au mashua, kutokana na asili yake, sio mahali pa ufikiaji rahisi au kwa watalii. Jiji lina mazingira rafiki kwa mapumziko ya baharini na kituo cha watalii," anasema Mirvari Gahramanli.

Hata hivyo,kutokana na kushuka kwa uzalishaji wa mafuta ambako miundo ya kisiwa hicho inaonekana kukumbana nayo, huenda kisiteuliwe kuwa kivutio cha watalii.

Kwa mujibu wa utafiti uliochapishwa katika Communications Earth & Environment ,kisiwa hiki kingeporomoka kwa mita 18 ifikapo 2100,ambapo ni sawa 34% ya Eneo la bahari.

Katika utafiti huo, wanasayansi walionya kuwa maji hayo yatashuka kati ya mita 9 na 18 ifikapo mwisho wa karne hii, ikiwa utoaji wa gesi chafu utaendelea katika viwango vya sasa.

Kwa sasa, kutpoka umbali wa kilomita chache tu, katika siku chache COP29 itajadili tena hali ya hewa ya sasa na ya baadaye ya dunia.

Tukio ambalo rais wake mteule, Mukhtar Babayev, alisema kuwa "juhudi za kila mtu" zitahitajika.

Unaweza pia kusoma

Imetafsiriwa na Martha Saranga na kuhaririwa na Yusuf Jumah