Netflix yashitakiwa kwa kuwachunguza watumiaji wake, wakiwemo watoto

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Liv McMahon
- Nafasi, Technology reporter
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Jimbo la Texas nchini Marekani limefungua kesi dhidi ya kampuni ya Netflix, likiiweka katika tuhuma nzito za kukusanya na kutumia taarifa ama data za watumiaji wake, ikiwemo watoto bila ridhaa yao ya wazi, na baadaye kutumia taarifa hizo kwa malengo ya kibiashara na uboreshaji wa huduma zake.
Kesi hiyo, iliyowasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Texas Ken Paxton, inadai kuwa Netflix imekuwa ikikusanya mabilioni ya taarifa kuhusu tabia za watumiaji wake. Taarifa hizo ni pamoja na kile wanachotazama, muda wanaokaa kwenye maudhui, na jinsi wanavyoingiliana na mfumo wa jukwaa hilo.
"Kila kinachofanywa na kwenye jukwaa hili kinageuzwa kuwa data inayoweza kumuanika mtumiaji," ofisi ya mwanasheria huyo inasema.
Texas inasema Netflix hapo awali ilijitangaza kama kampuni inayoheshimu faragha ya watumiaji wake, tofauti na kampuni nyingine kubwa za teknolojia, lakini sasa inadaiwa kuwa ilitumia mbinu mbalimbali za kuwafanya watumiaji waendelee kutumia muda mwingi kwenye jukwaa hilo. Miongoni mwa mbinu hizo ni kipengele cha auto-play, ambacho huanza kucheza maudhui moja kwa moja bila mtumiaji kubofya.
Aidha, inadaiwa kuwa kampuni hiyo ilianza kushirikiana na wahusika wa biashara ya data , hatua ambayo ilisaidia kuongeza mapato yake kwa kiwango kikubwa kupitia uchambuzi wa tabia za watumiaji.
Netflix imekanusha vikali madai hayo, ikisema kesi hiyo haina msingi na inategemea taarifa zisizo sahihi na zilizopotoshwa. Kampuni hiyo imesisitiza kuwa inazingatia sheria za ulinzi wa data katika maeneo yote inakofanya kazi na kwamba inaheshimu faragha ya watumiaji wake.

Chanzo cha picha, Getty Images
"Kwa heshima ya jimbo kubwa la Texas na Mwanasheria Mkuu Paxton, kesi hii haina msingi na inategemea taarifa zisizo sahihi na zilizopotoshwa," msemaji wa Netflix aliiambia shirika la habari.
"Netflix inachukulia kwa uzito faragha ya watumiaji wetu na inazingatia sheria za faragha na ulinzi wa data kila mahali tunapofanya kazi."
BBC imewasiliana na Netflix ili kupata maoni.

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
"Unapotazama Netflix, Netflix pia inakutazama wewe," inasema kesi iliyowasilishwa Jumatatu wiki hii na Mwanasheria Mkuu wa Texas.
Kwa mujibu wa hati hiyo ya mashtaka, Neflix maarufu kwa filamu ilijitangaza kuwa tofauti na makampuni mengine makubwa ya teknolojia katika namna inavyoshughulikia data na kuwatangazia watumiaji wake.
Inamnukuu mkuu wa zamani wa kampuni hiyo, Reed Hastings akiwa amesema mwaka 2019 na 2020 kwamba Netflix haikusanyi wala haitauza data za watumiaji, kama vile kuuza matangazo.
Lakini hati hivyo inasema Netflix ilitumia mchanganyiko wa mbinu za "kuvutia kupita kiasi" (addictive) kama vile kuchezesha maudhui kiotomatiki (auto-play), na "ukusanyaji mkubwa wa kumbukumbu" za shughuli za watumiaji ili kuwafanya watu waendelee kutumia tovuti.
Kati ya matukio mabilioni yaliyorekodiwa ni pamoja na kile ambacho watumiaji walibofya na kukitazama wakati gani, na walikaa kwa muda gani, hati hiyo ya mashtaka inaongeza.
Hati hiyo inasema Mwaka 2022, kampuni pia ilianza kutumia data zilizokusanywa kimya kimya kutoka kwa watoto na familia ilizowafanya kubaki wakitazama skrini zao" na kutumia kibiashara ili kusaidia kuongeza mapato ya mabilioni ya dola.
"Kwa kifupi, Netflix iliuza usajili wa maudhui yake kama njia ya kuepuka ufuatiliaji, lipa kila mwezi, epuka kufuatiliwa," kesi hiyo inasema.
"Watu wa Texas waliamini makubaliano hayo. Netflix ilikiuka ikijenga mfumo uleule wa ukusanyaji data ambao watumiaji walikuwa wanalipa ili kuukwepa."
Afrika Mashariki iko salama?

Chanzo cha picha, Getty Images
Ingawa kesi hii inatokea Marekani, mjadala wake unaathari pana zaidi duniani, ikiwa ni pamoja na Afrika Mashariki, ambako matumizi ya Netflix na majukwaa mengine ya kutazama video na filamu (streaming) kama YouTube, Showmax na Disney+ yanaendelea kuongezeka kwa kasi.
Afrika Mashariki iko salama? Swali hili linazidi kuibuka miongoni mwa wataalamu wa teknolojia na watumiaji, hasa kutokana na ukweli kwamba huduma nyingi za kidijitali zinazotumika katika kanda hii hutegemea mifumo ya kukusanya na kuchambua data za watumiaji ili kuboresha huduma na matangazo.
Katika miji kama Dar es Salaam, Nairobi, Kampala na Kigali, vijana ndio watumiaji wakubwa wa huduma hizi, lakini wengi hawasomi kwa kina sera za faragha (privacy policies) kabla ya kutumia majukwaa hayo. Hali hii inaleta mjadala kuhusu kiwango cha uelewa wa watumiaji kuhusu kile kinachofanyika nyuma ya pazia la "burudani ya kidijitali".
Wataalamu wa teknolojia wanasema kuwa ingawa huduma hizi kwa ujumla zinazingatia sheria za kimataifa za ulinzi wa data, changamoto kubwa katika nchi za Afrika Mashariki ni elimu ndogo ya kidijitali kwa watumiaji kuhusu jinsi data zao zinavyokusanywa na kutumiwa.
Vitu kama 'auto-play, mapendekezo ya maudhui (recommendations), na kufuatilia kile mtumiaji anachotazama kwa muda mrefu ni sehemu ya mifumo ya kawaida ya majukwaa haya, lakini pia vinachangia kiasi kikubwa cha data kinachokusanywa kila siku.












