Marekani inaweza kuisaidia Iran? Wairan wenyewe wanasemaje?

Waandamanaji wa Irani wanakusanyika karibu na magari yanayowaka barabarani huko Tehran, Iran mnamo Januari 8.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

Maelezo ya picha, Waandamanaji wa Irani wanakusanyika karibu na magari yanayowaka barabarani huko Tehran, Iran mnamo Januari 8.
Muda wa kusoma: Dakika 6

Kwa Mojdeh na mumewe, swali la uingiliaji wa Marekani nchini Iran si la kisiasa tu, ni la kibinafsi kabisa.

Mwanzoni mwa mwezi Januari, walisafiri kutoka makazi yao Washington, DC kwenda Tehran kuwatembelea familia, wakitarajia safari fupi na ya kawaida. Badala yake, maandamano yalizuka, safari za ndege zikafutwa, na wakajikuta wamekwama katika jiji ambacho hakikuwa tena na utulivu wala uhakika.

"Maisha yalikuwa kama yamesimama," alisema Mojdeh, hasa nyakati za usiku ambapo intaneti na hata mitandao ya simu vilikatika.

Hawakuwa wamepanga kuandamana. Lakini usiku wa tarehe 7 na 8 Januari, alisema, haikuwezekana kubaki pembeni.

"Ukitoka nje ya nyumba yako, ulikutana na maandamano," alisema. BBC imebadilisha jina lake halisi kwa ajili ya kulinda utambulisho wake na wa mumewe.

Jioni moja, baada ya kula katika mgahawa, walipotoka nje walikuta mji umebadilika kabisa: umati wa watu ulikuwa umejaa mitaani, na katika baadhi ya maeneo vikosi vya usalama vilionekana kupoteza udhibiti.

"Ilionekana kana kwamba watu wameiteka Tehran," alisema.

Maandamano yalilipuka kote Iran muda mfupi kabla ya mwaka mpya, yakichochewa na hasira dhidi ya ugumu wa maisha na kushuka kwa thamani ya sarafu. Hata hivyo, haraka yakageuka kuwa wito wa kumaliza utawala wa Jamhuri ya Kiislamu. Siku chache baadaye, vikosi vya usalama vilijibu kwa kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji.

Idadi halisi ya waliokufa ni vigumu kuthibitisha kutokana na kukatwa kwa intaneti nchini Iran na ukosefu wa taarifa huru. Shirika la Human Rights Activists News Agency (HRANA) lenye makao Marekani limesema limethibitisha vifo vya waandamanaji zaidi ya 6,000, huku Iran Human Rights yenye makao Norway ikisema huenda idadi ya mwisho ikazidi 25,000. Mamlaka za Iran zimesema watu wasiopungua 3,117 waliuawa, lakini zimedai wengi wao walikuwa wanachama wa vikosi vya usalama au raia waliokuwa wakitazama matukio, na kulaumu vifo hivyo kwa "waandamanaji."

Mwandamanaji akiwa na ishara wakati wa maandamano nje ya Ubalozi wa Iran mjini London tarehe 14 Januari.

Chanzo cha picha, LightRocket via Getty Images

Maelezo ya picha, Mwandamanaji akiwa na ishara wakati wa maandamano nje ya Ubalozi wa Iran mjini London tarehe 14 Januari.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Rais wa Marekani, Donald Trump, amerudia mara kadhaa kuonyesha kuunga mkono waandamanaji wa Iran.

Ijumaa, maafisa wa Marekani na Iran walifanya mazungumzo, ingawa matarajio yalikuwa madogo. Akiwa ndani ya ndege ya Air Force One baadaye siku hiyo, Trump alisema mazungumzo yalikuwa "mazuri sana" na kwamba Iran "inaonekana kutaka kufikia makubaliano kwa dhati."

Sauti ya Mojdeh ilitetemeka alipoelezea hali ya nchi yake wakati wa maandamano: watu wakikimbia, wakipiga kelele, wakipigwa, kumbukumbu zilizobaki moyoni mwake hata baada ya kufanikiwa kuondoka Iran.

Mumewe alishtushwa na jambo jingine: miongoni mwa marafiki na familia nchini Iran, wazo la kuhusika kijeshi kwa Marekani halikuonekana kama shambulio, bali kama "msaada."

Wakiwa wanaishi salama Marekani, wanatambua hali ya kukata tamaa iliyopo, lakini wanabaki na mashaka iwapo hatua kama hiyo ingeweza kuleta kile ambacho waandamanaji wanakitaka kwa dhati si tu mabadiliko ya utawala, bali pia heshima, usalama wa kiuchumi na uhuru.

Kwa kutazama kwa mbali, wana hofu juu ya gharama ya kuchanganya uharibifu na ukombozi.

Waandamanaji wa Iran walifunga barabara na kuwasha moto karibu na bango iliyopakwa rangi na kauli mbiu "Kifo kwa Dikteta" wakati wa maandamano huko Shiraz, Iran, tarehe 9 Januari.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

Maelezo ya picha, Waandamanaji wa Iran walifunga barabara na kuwasha moto karibu na bango iliyopakwa rangi na kauli mbiu "Kifo kwa Dikteta" wakati wa maandamano huko Shiraz, Iran, tarehe 9 Januari.

"Mabadiliko ya utawala yanapaswa kutoka ndani"

Wiki kadhaa baada ya ukandamizaji wa maandamano na kunyimwa kwa intaneti, Wairani walioko ndani na nje ya nchi bado wanatafakari iwapo Marekani inapaswa kuingilia kati.

Shirin, Muirani-Mmarekani anayeishi California, alisema bado ana matumaini ya uingiliaji wa kigeni.

"Iwapo jumuiya ya kimataifa kweli inataka kukomesha ghasia na kuzuia kuyumba zaidi kwa dunia, hatua zinahitajika," alisema Shirin, mwenye umri wa miaka 52, aliyeomba jina lake la ukoo lisitajwe kwa hofu ya usalama wa familia yake nchini Iran.

"Kichwa cha nyoka kisipokatwa, sumu huenea zaidi ya mipaka, zaidi ya kanda, zaidi ya vizazi."

Hata hivyo, baadhi ya Wairani wana hofu kuwa uingiliaji huo unaweza kuwaumiza wapendwa wao waliobaki chini ya utawala huo.

Roozbeh Farahanipour, aliyewahi kufungwa Iran kwa harakati za wanafunzi na sasa ni mmiliki wa mgahawa Los Angeles, aliiambia BBC kuwa ana "wasiwasi wa kudumu" kuhusu uwezekano wa Marekani kuingilia kati.

"Sijui ni wangapi wameuawa, wangapi wamejeruhiwa, au nani amepotea. Sijui jinsi ya kuwafikia mama, baba, kaka, dada, wake, waume au watoto kuwapa pole na kuonyesha mshikamano," alisema.

Alisema msaada wa kimataifa unahitajika, lakini anakumbuka hatari na historia ya uingiliaji wa Marekani. Mwishowe, mabadiliko ya utawala yanapaswa kutoka ndani.

"Leo, nguvu kubwa zaidi iko katika umoja, nidhamu, azma na uhamasishaji wa umma kwa wingi, kujenga umati mkubwa na kuyahimiza waliobaki kwa mfumo kujiunga na harakati za wananchi. Kuporomoka kwa ndani kuna uzito mkubwa zaidi kuliko nguvu yoyote ya nje," alisema Farahanipour.

"Hakuna njia nyingine"

Ali, mwenye miaka 43, alizaliwa Iran na ameishi Marekani kwa miaka 21.

Kwa muda mrefu aliunga mkono mageuzi ndani ya mfumo wa kisiasa wa Iran na mara nyingi alipigia kura wagombea wa wastani nchini Marekani. Karibu mwaka 2014, alisema alikata tamaa.

"Tumeona hili kabla," alisema akirejelea maandamano, ahadi na ukandamizaji wa mwaka 2009 na kabla yake. Aliomba jina lake la mwisho lisitajwe.

Kila mara, alisema, watu waliuawa na hakuna kilichobadilika kwa kiasi kikubwa. Kwa mtazamo wake, utawala hauwezi kurekebishwa na bila shinikizo la nje, hauwezi kushindwa.

Haitishi uvamizi kamili, bali mashambulizi ya kulenga miundombinu ya serikali na viongozi wakuu, si raia. Alisisitiza kuwa kushambulia utawala kwa ombi la wananchi wake ni tofauti na kushambulia nchi moja kwa moja.

Wengi anaowajua nchini Iran sasa wanataka aina fulani ya uingiliaji wa Marekani si kwa sababu wana imani na nia za Marekani, bali kwa sababu hawaoni njia nyingine.

Hemad Nazari, mwanaharakati na mpiga picha wa Iran aliyeondoka nchini humo mwaka 2015 na sasa anaishi Denmark, anaunga mkono mtazamo huo.

"Tutawezaje kujadiliana na utawala huu?" alihoji Nazari, mwenye miaka 36.

Alisema uingiliaji wa kigeni unaweza kubadili mizani ya nguvu. "Wakati bora wa kuingilia ulikuwa mwezi mmoja uliopita. Wakati wa pili bora ni sasa."

Nazari, ambaye hahusiani na shirika au chama chochote cha kisiasa, alianzisha mtandao wa kusambaza simulizi za moja kwa moja kutoka Iran, hasa wakati wa maandamano na kukatika kwa intaneti. Wakati wa kukatika, watu walimtumia ujumbe kupitia njia mbadala kama Starlink, naye akasambaza taarifa hizo kwenye mitandao yake ya kijamii, ikiwemo X ambako ana wafuasi zaidi ya 21,000.

Kutokana na ukuaji wa mtandao huo tangu 2019, alisema hawezi kurudi Iran kwa hofu ya kukamatwa.

Katika wiki chache zilizopita pekee, amepokea zaidi ya jumbe 500 za moja kwa moja.

Watu anaowasiliana nao nchini Iran wanaamini uingiliaji ndio chaguo pekee.

"Wanasema, 'Tulienda mitaani. Tukauawa. Hakuna njia nyingine.'"

Aliongeza kuwa wengi wanaamini hata kama raia wanaweza kupoteza maisha, bila uingiliaji, hakuna kitakachobadilika.

Mwandamanaji akiwa amebeba bango lenye kauli mbiu 'Free Iran. Dijitali yazima Iran' wakati wa maandamano huko Madrid, Uhispania

Chanzo cha picha, Europa Press via Getty Images

Maelezo ya picha, Mwandamanaji akiwa amebeba bango lenye kauli mbiu 'Free Iran. Dijitali yazima Iran' wakati wa maandamano huko Madrid, Uhispania

Wasiwasi kuhusu watu milioni 90

Hata kama maandamano yamepungua, ukandamizaji unaendelea kwa njia nyingine.

Iran Human Rights (IHRNGO), shirika lisiloegemea upande wowote, linakadiria kuwa watu wasiopungua 40,000 wamekamatwa tangu maandamano yaanze. Limesema lina "wasiwasi mkubwa" kuhusu hali ya waliopotea au kuzuiliwa, wakiwemo waliokosa ruhusa ya kupata mawakili na wengine wanaoshikiliwa mahali pasipojulikana.

IHRNGO na HRANA zimesema zimepokea taarifa kuwa vikosi vya usalama vinafanya uvamizi katika vituo vya afya na kuwakamata wahudumu waliowasaidia waandamanaji waliojeruhiwa. Hata hivyo, HRANA imenukuu mkuu wa Baraza la Madaktari la Iran akisema "hakuna daktari aliyekamatwa kwa kuwahudumia waandamanaji."

Huduma za intaneti zimeanza kurejea kwa sehemu, lakini huduma nyingi bado haziaminiki au zimezuiwa.

Kwa Wairani wa ndani na nje ya nchi, mjadala kuhusu uhusika wa Marekani si wa kinadharia tena. Umejengwa juu ya huzuni, hofu na uchovu na hisia inayoongezeka kwamba muda huenda unaisha.

"Ni vigumu kutazama matukio ya mwezi uliopita ukiwa mbali hivi," alisema Shirin.

"Inauma kama Muirani, lakini pia kama binadamu. Na si kuhusu familia zetu tu tunawahofia watu milioni 90."

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid